Mifuko ya Pensheni

Hifadhi ya Jamii ni mfumo ambao jamii husika hujiwekea kwa lengo la kujikinga dhidi ya majanga yasiyotarajiwa. Majanga hayo ni kama Maradhi, Ulemavu, Kupoteza kazi, Kuacha kazi kwa sababu ya uzee (kustaafu).

Sera ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii

Nchini Tanzania mfumo wa Hifadhi ya Jamii umegawanyika katika nguzo kuu tatu (3), ambazo ni:

 • Nguzo ya kwanza – Nguzo hii inahusisha Hifadhi ya Jamii katika mfumo wa huduma za kijamii zinazogharamiwa kwa kodi ya  Serikali, mashirika ya wahisani wa ndani na nje na taasisi za kijamii
 • Nguzo ya pili – Katika nguzo hii, Hifadhi ya Jamii inahusisha uchangiaji wa lazima kwa wenye kipato na walio katika ajira. Hii ndio nguzo ambayo Mifuko ya Hifadhi ya Jamii inahusika. Uchangiaji katika mifuko hiyo ugharamiwa kwa pamoja kati ya Waajiri pamoja na Wafanyakazi.
 • Nguzo ya tatu – Hifadhi ya Jamii katika nguzo hii hutolewa kwa mfumo uchangiaji wa hiari ambao unawalenga zaidi watu wenye kipato cha ziada na huchangia kama ziada baada ya kutekeleza majukumu ya kisheria kwenye nguzo ya pili.

Mfuko wa Pensheni

Mfuko wa pensheni ni uwekezaji wa mali unaolenga kuzalishaji na  ukuaji wa uchumi imara kwa muda mrefu, na kutoa pensheni kwa wafanyakazi pindi watakapofika ukomo wa kufanya kazi  na kuanza maisha ya kustaafu.

Mifuko ya Pensheni Nchini Tanzania

Tanzania Bara kuna Mifuko ya pension ya lazima miwili nayo ni;

 • Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF)
 • Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF)

Kwa ujumla Mfuko hii yote husajiliwa na kusimamiwa na Mamlaka ya Usimamizi na udhibiti wa sekta ya hifadhi ya jamii

Umuhimu wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii.

 • Kuongeza wigo wa Hifadhi ya Jamii (Social Security Coverage)
 • Kupunguza umasikini kwa Watanzania
 • Kuongeza kinga kwa Watanzania katika Nyanja kama vile elimu, afya, uzazi, ulemavu na uzee.
 • Kuongeza uwekezaji na kutoa fursa kwa Wajasiriamali kupitia vikundi mbalimbali vya kijamii
 • Kuchangia maendeleo ya miradi mbalimbali ya Serikali
 • Kuongeza ajira kwa Watanzania kupitia miradi inayoendeshwa na Mifuko hiyo

Mafao yanayotolewa

Kuna aina mbili za mafao yatolewayo na mifuko ya hifadhi za jamii Tanzania;  mafao ya muda mrefu na muda mfupi

Mafao ya Muda Mrefu

 • Pensheni ya Uzeeni – kustaafu
 • Pensheni ya Ulemavu
 • Pensheni ya Urithi (kifo)

Mafao ya Muda mfupi

 • Uzazi – kwa baadhi ya mifuko
 • Kuumia kazini – kwa baadhi ya mifuko
 • Afya – kwa baadhi ya mifuko
 • Msaada wa mazishi
 • Elimu – mfuko mmoja

Uhusika wa sekta isiyo rasmi kwenye Mifuko ya hifadhi ya Jamii

Sekta isiyo rasmi inahusika katika Mifuko isiyo rasmi kwa kujiunga kwenye mfumo wa huchangiaji wa hiyari unaratibiwa na Mifuko ya pensheni.lakini pia sheria inawapa uhuru wa kuanzisha mifuko ya hiari kwenye sehemu au makundi yao ya kazi na kuisaji kwa mamlaka.

Kutoa Miongozo

Mamlaka imeundwa kwa Sheria Na. 2 ya mwaka 2018, Sura ya 135. Kwa mujibu wa marekebisho yaliyofanyika katika Sheria ya SSRA, Miongozo (Guidelines) yote iliyotengenezwa chini ya Sheria hiyo inapaswa kutangazwa katika Gazeti la Serikali ambayo ilitangazwa tarehe 3 mwezi Agosti, 2018.

Mamlaka ina jukumu la kulinda, kutetea na kuendeleza maslahi ya wanachama wa sekta ya Hifadhi ya Jamii.  Kifungu cha 5 (1) (c) cha Sheria ya Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Hifadhi ya Jamii kinampa Mkurugenzi Mkuu mamlaka ya kutoa miongozo, Mamlaka imetoa miongozo 14 inayolenga kuhakikisha kuwa sekta inakuwa bora na endelevu na hivyo kuboresha maisha ya wanachama na kuchangia maendeleo ya Taifa letu kwa ujumla. Miongozo ambayo mamlaka imeitoa mpaka sasa ni;

 • Muongozo wa Uendeshaji Bodi ya Wadhamini wa Mifuko, 2018  
 • Muongozo wa Taarifa za Tathmini za Mifuko ya Hifadhi ya Jamii, 2018
 • Muongozo wa Uandikishaji Wanachama, 2018
 • Muongozo wa Usalama wa Taarifa za Kielektroniki ,, 2018
 • Muongozo wa Kujumlisha Vipindi Vya Uchangiaji , 2018
 • Muongozo wa Uwekezaji, 2018
 • Muongozo wa Utunzaji wa Kumbukumbu na Takwimu, 2018
 • Muongozo wa Usimamizi wa Vihatarishi, 2018
 • Muongozo wa Matumizi ya Fedha za Mifuko, 2018
 • Muongozo wa  Utengamo wa Mifumo ya TEHAMA, 2018
 • Muongozo wa Usalama wa Taarifa za Kielektroniki , 2018
 • Muongozo wa Kuandaa Taarifa za Mwaka, 2018
 • Muongozo wa Ukwasi wa Mifuko,2018
 • Muongozo wa Mfuko Mtambuka,2018

Vyama vya Wafanyakazi vyaridhiswa na ushirikishwaji katika zoezi la kuunganisha mifuko ya hifadhi ya jamii

“Mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni! Katika zoezi hili la kuunganisha mifuko sisi vyama vya wafanyakazi tumeshirikishwa kwa kiwango kikubwa sana, tumeshirikishwa kuanzia hatua za maoni mpaka kwenye vikao vya maamuzi hivyo matokeo ya kuunganishwa kwa mifuko ni juhudi zetu sisi sote kama vyama vya wafanyakazi, vyama vya waajiri na serikali kwa pamoja” hii ni kauli ya Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA), Ndugu Tumaini Nyamhokya wakati akitoa neno la utangulizi kwenye semina ya Hifadhi ya Jamii iliyoandaliwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) kwa wajumbe wa Baraza Kuu la Tucta jijini Dodoma.

Kumekuwepo na maoni mbalimbali kutoka kwa wadau juu ya namna zoezi hili la kuunganisha mifuko ilivyoendeshwa, wengine wakihoji ushirikishwaji wa  wafanyakazi, lakini ndugu zangu niwatoe wasiwasi sisi kama viongozi wenu tumeshirikishwa kikamilifu, tulienda kwenye vikao tukiwa na maoni yetu lakini wenzetu upande wa Serikali wakaja na hoja nzito zenye namba hivyo ikatupasa kukubaliana katika mambo ya msingi kwa mstakabali wa wanachama wetu ambao ndio wanufaika wa mifuko hii ya Hifadhi ya Jamii. Anasisitiza Ndugu Nyamhokya.

Ndugu Nyamhokya alisema Mifuko hii ya Hifadhi za Jamii ni ya wafanyakazi wenyewe kwa maana michango ya wafanyakazi ndio inayojenga mfumo huu, hivyo wenye uwezo wa kujenga na kuendeleza au kubomoa ni wafanyakazi wenyewe. Natambua kuwa wafanyakazi walikuwa na matumaini ya kupata pensheni kubwa zaidi lakini haikuwezekana kwasababu mifuko yetu haina uwezo wa kulipa viwango hivyo kwa sasa, hivyo nitoe rahi kwa wafanyakazi nchini kupokea hiki kilichopo leo kwani hata hapa tulipofikia ni pazuri ukilinganisha na tulipotoka na ata wenzetu wa nchi jirani wanatamani kufika hapa tulipo.

Tusiingie kwenye mtego wa wenzetu waliotutangulia kujiwekea mafao makubwa kuzidi uwezo wa mifuko kulipa kwani ndio iliyotufikisha hapa kwa baadhi ya mifuko kushindwa kutekeleza wajibu wao kwa wakati, ni bora tupokee kidogo kinachokidhi mahitaji kuliko kikubwa kitakachoua mifuko yetu.  Anasisitiza Ndugu Nyamhokya

Mkurugenzi Mkuu wa SSRA, Dkt. Irene Isaka na Viongozi Waandamizi wa TUCTA wakiimba kwa pamoja wimbo wa maarufu wa Mshikamano wakati wa Semina ya Hifadhi ya Jamii kwa Wajumbe wa Baraza Kuu la TUCTA, Jijini Dodoma

Akizungumza katika Semina hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa SSRA, Dkt. Irene Isaka alisema SSRA inatambua kuwa ajenda ya kufanya mabadiliko katika sekta ya Hifadhi ya Jamii toka mwanzo ilikuwa ni ajenda ya vyama vya wafanyakazi na  ndio maana kwa kila hatua tuliyofanya tunajitaidi kuwashirikisha ili muweze kufahamu mabadiliko hayo. Hii ni kwa sababu tunatambua kuwa vyama vya wafanyakazi ni wadau muhimu katika sekta ya Hifadhi ya Jamii na mtaweza kutusaidia katika kuwahabarisha wanachama wenu na watanzania kwa ujumla.

Dkt. Irene Isaka alifafanua kwamba hatua hii ya kuunganisha mifuko ililenga mambo makubwa mawili. Moja ni kukidhi kilio cha muda mrefu cha wafanyakazi kuhusu kuunganisha Mifuko ya Pensheni ili kupunguza gharama za uendeshaji, kuondoa ushindani usio na tija baina ya Mifuko ya pensheni ambayo kimsingi ilikuwa inatoa mafao yanayofanana, kupunguza migogoro baina ya Mifuko, kuimarisha uwiano wa idadi ya wanachama wachangiaji na wastaafu na pili ni kuboresha mafao ya wanachama, kuongeza tija katika Sekta ya Hifadhi ya Jamii na kukuza uchumi wa nchi kwa ujumla.

Kama nilivyotangulia kusema hapo  awali uwepo wenu  mahali hapa leo kutasaidia kupata uelewa wa mabadiliko na maboresho yalifanyika kwa kina ili kama wadau muhimu mkatumie nafasi zenu kuwahabarisha na kuwaelimisha wanachama wetu na wananchi kwa ujumla. Aidha, ni imani yangu kwamba baada ya semina hii  mtakwenda kuwa mabalozi wazuri wa mabadiliko na maboresho haya yaliyofanywa na Serikali kwa nia njema. Alisema Dkt. Irene Isaka.

Akitoa neno la shukrani, Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA) Ndugu Tumaini Nyamhokya alisema SSRA imekuwa ni kiungo kizuri kati ya Serikali na vyama vya wafanyakazi katika kutetea na kulinda maslahi ya wafanyakazi ambao ni wanachama wa mifuko ya hifadhi ya jamii, kwa nyakati tofauti tumekaa pamoja na SSRA tukichambua na kujadiliana kuhusu namna bora ya kuboresha sekta ya hifadhi ya jamii nchini.

Baadhi ya Wajumbe wa Baraza Kuu la TUCTA wakifuatilia kwa makini Semina ya Hifadhi ya Jamii iliyoandaliwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) Jijini Dodoma

SSRA yatoa Elimu ya Hifadhi ya Jamii kwa Baraza la Wazee Taifa

Wazee kutoka sehemu mbalimbali nchini kupitia Baraza lao la Taifa wameiomba Serikali na wadau wanaohusika kuharakisha mchakato wa upatikanaji wa pensheni Jamii kwa wazee ili kukabiriana na changamoto ya umaskini wa kipato unawakabiri wazee walio wengi nchini. Maombi hayo yamewasilishwa wakati wa Semina ya Hifadhi ya Jamii iliyoendeshwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) kwenye kongamano la Wazee lililofanyika tarehe 30/09/2018 katika ukumbi wa mikutano wa AICC, Jijini Arusha,

Akiwakilisha maombi hayo Mwenyekiti wa Baraza la Wazee Taifa, Mzee Sebastian Bulegi alisema kwa kipindi kirefu wamekuwa wakiiomba bila mafanikio kuhusu Pensheni Jamii kwa Wazee, hivyo wanatumia Kongamano hili kama jukwaa la kufikisha kilio chao kwa mara nyingine.

Aidha, wazee hao wameiomba serikali kuwaongezea kima cha chini cha pensheni ya mwezi ili waweze kujikimu kimaisha

SSRA yawaelimisha Waajiri kuhusu mabadiliko ya Sekta za Hifadhi ya Jamii

Mamlaka ya Usimamizi wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) imekutana na waajiri nchini kwa lengo la kuwaelimisha kuhusu mabadiliko ya sheria za Hifadhi ya Jamii. Semina hiyo iliyoandaliwa na SSRA kwa kushirikiana na Jumuiya ya Waajiri nchini (ATE) ilifanyika tarehe 03/10/2018 katika ukumbi wa mikutano wa Sea Cliff, jijini Dar es Salaam na kushirikisha jumla ya wajumbe 105.

Katika semina hiyo pamoja na mambo mengine walipata fursa ya kuelimishwa kuhusu sheria ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa umma, sheria ambayo inaunganisha Mifuko ya Pensheni minne (4) ya PSPF, LAPF, PPF na GEPF na kuunda Mfuko mmoja kwa ajili ya Watumishi wa Umma yaani PSSSF. Sambamba na kuanzishwa kwa Mfuko huo, Sheria hii imefanya marekebisho kwenye Sheria ya Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii, (The National Social Security Fund) Sura ya 50 ili kuufanya Mfuko wa NSSF kuwa Mfuko utakaohudumia wafanyakazi wa Sekta Binafsi na Sekta isiyo rasmi. 

Akizungumza katika semina hiyo mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu, Bwana Joseph Mutashubirwa ambae ni Mkurugenzi wa Utafiti, Tathimini na Sera kutoka SSRA alisema elimu kwa waajiri kutasaidia kupata uelewa wa mabadiliko na maboresho yalifanyika ili kama wadau muhimu mkatusaidie katika utekelezaji wa sheria hizi lakini pia mkatumie nafasi zenu kuwahabarisha na kuwaelimisha wanachama kwa ujumla.

Aidha, ni imani yangu kwamba baada ya kikao hiki mtakwenda kuwa mabalozi wazuri wa mabadiliko na maboresho haya yaliyofanywa na Serikali kwa nia njema. Alisisitiza Bwana Mutashubirwa.

Katika Semina hiyo Waajiri wameimizwa kutekeleza wajibu wao kwa wakati ili kubiresha huduma zinazotolewa na mifuko ikiwa ni pamoja na ulipwaji wa mafao kwa wakati.

Tovuti Muhimu